BE FORWARD.JP

BE FORWARD.JP
JAPANESE CAR EXPORTER

Wednesday 17 July 2013

Maandamano kupinga kodi ya simu yanukia


Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika,  amesema amewasilisha kwa Katibu wa Bunge, kusudio la kupinga tozo ya kodi ya simu kwa wamiliki wa kampuni za simu za mkononi nchini.

Mnyika aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuwa aliwasilisha kusudio lake hilo Julai 15 mwaka huu ili kufutwa kwa kifungu kinachoidhinisha kampuni hizo kutozwa kodi hiyo.

“Katika barua hiyo nimeomba masharti ya kanuni ya 21(1) (d) (e) na (2) ya kanuni za kudumu za Bunge yazingatiwe kuniwezesha kuchukua hatua hiyo katika mkutano wa 12 wa Bunge,” alisema Mnyika.

Alisema mpango wake huo umekuja baada ya Bunge kupitisha Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2013, ambayo pamoja na mambo mengine imeidhinisha tozo ya kodi hiyo.

Alisema muswada huo ulifanya marekebisho ya Sheria ya ushuru wa bidhaa  na kuanzisha ushuru wa bidhaa kwa kadi za simu kwa mmliki wa simu za kiganjani.

Mnyika alisema miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa na wananchi ni kukusanya saini za wananchi kupinga kodi hiyo na kuwasilisha bungeni au kwa serikali.

“… wananchi wamependekeza yatajwe majina ya wabunge waliotoa mawazo ya waliopendekeza kodi hiyo,” alisema Mnyika.

Alisema pia wananchi wamependekeza kufanyika kwa maandamano ya kupinga kupitishwa kwa kodi hiyo ya simu kwa wamiliki wa kampuni hizo na kutaka utekelezaji wa utozaji wake kusitishwa.

Mnyika alisema vilevile wananchi walitaka hatua hizo zisiwe kwa kodi hiyo ya simu peke yake bali zote zenye kuongeza ugumu na gharama za maisha kwao.

Aidha alisema kuwa ameanza kuchukua hatua katika mapendekezo yaliyotolewa kwa kukusanya zaidi ya saini 23,569 kupitia mikutano yake ya hadhara na kwa njia nyingine.

“Tayari nimeanza utekelezaji wa mapendekezo na ninatoa wito kwa kila mwananchi aliyeguswa na suala hili kwa kutumia haki yake kwa kuzingatia wajibu ni muhimu kuwezesha utekelezaji wa hatua hizi kuendelea,” alisema.

Kodi hizo zilianza kutozwa na serikali mwanzoni mwa Julai, mwaka huu hivyo kuwalazimu wamiliki wa simu nchini kuingia gharama zaidi kwa asilimia 14.5 ili kuongeza mapato yake na kugharamia elimu.

Akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2013/14 bungeni hivi karibuni, Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa alisema kodi hizo zingeanza kutozwa  Julai 1, mwaka huu.

Dk. Mgimwa alisema kuwa kama chanzo kipya cha mapato ya Serikali, inakusudia kutoza ushuru kwenye huduma zote za simu za mkononi badala ya muda wa maongezi peke yake.

Alifafanua kuwa ushuru wa asilimia 2.5 utatumika kugharimia elimu nchini kwa kuzingatia mapendekezo ya Kamati Maalumu ya Spika ya Kushauri kuhusu mapato na matumizi ya Serikali.

Vilevile alitangaza kuanzisha kodi ya zuio ya asilimia 10 ya kamisheni ya usafirishaji wa fedha kwa njia ya simu za mkononi ambazo zitakusanywa na kampuni za simu kutoka kwa wakala wanaotoa huduma hizo kupitia simu za mkononi.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, mapendekezo hayo ni utekelezaji wa ushauri wa Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) itafute vyanzo vipya vya kodi ili kuongeza mapato ya Serikali.

Naibu Spika, Job Ndugai alipotafutwa na NIPASHE kwa njia ya simu jana ili kuzungumzia suala hilo alisema  bajeti ikipitishwa inakuwa si rahisi kutenguliwa kwa kuwa ilipitishwa kwa maoni ya wabunge wote na kwamba baada ya kupitishwa kuna sheria zinazolinda hayo mafungu yaliyopitishwa.

Alizitaja baadhi ya sheria zinazolinda mafungu yanayopitishwa wakati wa kujadili  bajeti kuwa ni pamoja na sheria ya fedha (Financial Act) na sheria ya matumizi ya fedha (Appropriation Act).

Ndugai alisema hata hivyo inategemeana na jambo husika na kanuni gani ya Bunge aliyosimamia mhusika kupinga bajeti hiyo.

Kwa mujibu wa Ndugai, mbunge iwapo ana jambo anapaswa kutumia au kusimamia kifungu husika cha kanuni na hapaswi kuwa nalo binafsi bali analipeleka kwa kamati zinazohusika ndani ya bunge kabla ya kulipeleka kwa wabunge wote kulitolea maoni au kulijadili.

Hata hivyo, katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 99, kifungu cha 1 na 2 (a) ( i ) inasema: "Bunge halitashughulikia na jambo lolote kati ya mambo yanayohusika na ibara hii isipokuwa kama Rais amependekeza kwamba jambo hilo lishughulikiwe na Bunge na pendekezo hilo la Rais liwe limewasilishwa kwenye Bunge na Waziri.”

Ibara hiyo inaendelea kufafanua kwamba: “Mambo yanayohusika na ibara hii ni pamoja na haya yafutayo: Muswada wa Sheria kwa ajili ya lolote kati ya mambo yafuatayo: Kutoza kodi kwa namna nyingine yoyote isipokuwa kupunguza…”

No comments: